Wasaidizi wa jinsia na ardhi wanaweza kusaidia - miaka saba ya WOLTS nchini Tanzania | Land Portal

Jamii nyingi za vijijini nchini Tanzania zina changamoto zinazofanana  kutokana na makampuni ya uchimbaji madini na wawekezaji. Nimejionea jinsi wanaume na wanawake ambao ni wasaidizi wa jinsia na ardhi wanavyoweza kusaidia.

Kwa muda wa miezi minane iliyopita nimekuwa nikizunguka katika jamii za kaskazini mwa Tanzania pamoja na wasaidizi wa jinsia na ardhi walionufaika kupitia mradi wa kimataifa wa Usalama wa Umiliki wa Ardhi kwa Wanawake (Women’s Land Tenure Security-WOLTS), ambao shirika la HakiMadini, linashirikiana na Mokoro ya Uingereza na People Centered Conservation-PCC ya Mongolia.

Walikuwa wakishirikisha kile walichojifunza kupitia programu ya mafunzo ya jinsia na ardhi kwa jamii nyingine, kuhusu sheria ya ardhi na haki za wanawake, na waliweza kuelimisha na kuhamasisha jamii zote tulizozitembelea.

Katika kila kijiji changamoto zilifanana; wawekezaji walikuwa wakija na karatasi za serikali na vibali vinavyowapa haki ya kutafuta rubi au madini mengine, na wanakijiji hawakujua ni haki gani walikuwa nazo kulinda ardhi na maisha ya jamii zao.

Msaidizi mmoja wa jinsia na ardhi, Peter, alikuwa akiwasihi wasiogope. Mwanaume wa Kimasai mwenye moyo mkunjufu na uzoefu wa miaka mingi kama kiongozi wa mila na mwenyekiti wa zamani wa kijiji, alikuwa amepata ujasiri zaidi baada ya kuchaguliwa na jamii yake kushiriki katika programu ya mafunzo kuhusu jinsia na masuala ya ardhi. Ana uwezo wa kuzungumza kwa urahisi kuhusu haki za jamii wakati wachimbaji wanapofika kwenye ardhi yao na kueleza taratibu sahihi za kufuata ili kuhakikisha kila mtu ananufaika na kwamba watu wanyonge hawadhulumiwi. Pia ana madokezo mazuri juu ya nini cha kufanya ikiwa wachimbaji wa madini wataanza ghafla kulima ardhi –jambo ambalo limetokea katika maeneo zaidi ya moja tuliyoyatembelea.

Msaidizi mwingine wa jinsia na ardhi, Sindooi, aliwavutia wanawake na wanaume kwa mtazamo wake wa kujiamini kuhusu haki za ardhi za wanawake. Akiwa mjane katika umri mdogo, Sindooi alikuwa ametumia ujuzi wake mpya aliopata kupitia programu ya mafunzo ya jinsia na ardhi ya WOLTS kupata urithi wake. Pia alichaguliwa na jamii yake kushiriki mafunzo na amekuwa mstari wa mbele na sauti inayoongoza kutetea haki za ardhi za wanawake na kupinga unyanyasaji wa kijinsia (GBV) wa kila aina.

Peter alimuunga mkono Sindooi, akizungumzia dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia na kushawishi utoaji wa haki kwa wajane na wanawake ambao hawana watoto. Akitolea mfano mti mkubwa uliowafunika washiriki wote kutokana na jua kali katika kijiji kimoja, aliona kwamba miti isiyo na matunda ingali na manufaa mengi kwa watu wa jamii hiyo.

Mimi mwenyewe kama mwanamke wa Kimasai, niliweza kuona kwamba Peter na Sindooi, na wasaidizi wetu wengine wa jinsia na ardhi, Milya na Rosa, hawakuwa wakieleza tu mambo ya kitaalamu kama vile sheria ya ardhi na dhana za jinsia, bali waliweza kuyatafsiri katika lugha ya kila siku ambayo watu wangeweza kuelewa. Na hawakuogopa kuzungumza juu ya masuala ambayo nisingeweza kamwe kuthubutu kuyaibua.

Kwa mfano, Sindooi alizungumza waziwazi kuhusu wanaume kuzitelekeza familia zao, na kuwa na mahusiano nje ya ndoa zao. Wake, alisema, walilazimika kuishi kama wajane ingawa waume wao walikuwa bado wangali hai. Alipokuwa akiongea, wanaume wengi walikuwa wakitazama chini, wakichukua ujumbe wake wenye uchungu. Tuliondoka tukihisi kwamba kumekuwa na uhusiano wa kweli na jamii.

Nimekuwa nikifanya kazi ya haki za ardhi na uchimbaji madini nchini Tanzania kwa miaka mingi, lakini mradi huu umenifungua macho kuona uwezekano wa wasaidizi wa jinsia na ardhi wa ndani ya jamii kufanya mabadiliko ya kweli. Kwa kuzipa jamii nafasi ya kujifunza kuhusu haki zao, na kisha kuchagua watetezi wao wenyewe, wanaonekana kuwezeshwa zaidi kuliko watu wa nje wanapokuja kwa safari fupi kutoa mafunzo au ushauri.

Kilichoanza kama mradi kuhusu haki za ardhi za wanawake pia kimekuwa zaidi. Masuala nyeti ambayo hayangezungumzwa nilipokuwa msichana, leo yanazungumzwa mbele ya wanaume na wanawake wa rika zote. Wasaidizi wapya wa jinsia na ardhi wanatambuliwa, na njaa ya maarifa katika jamii itawasukuma mbele zaidi. Kuondoka kwenye vijiji tulivyotembelea pamoja na wasaidizi wa jinsia na ardhi, nina imani kuwa mabadiliko ambayo jamii inataka yataendelea kwa muda mrefu.

 

Joyce Ndakaru anafanya kazi kama Afisa Jinsia katika Shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania, HakiMadini. Yeye ni kiongozi wa timu ya mradi wa kimataifa wa WOLTS nchini Tanzania, ambao unatekelezwa na HakiMadini pamoja na Mokoro Ltd, shirika lisilo la kutengeneza faida lenye makao yake makuu nchini Uingereza. Kwa taarifa zaidi kuhusu WOLTS na upatikanaji wa ripoti za utafiti na machapisho, tafadhali tembelea http://mokoro.co.uk/project/womens-land-tenure-security-project-wolts/

Blogu hii ilichapishwa pia kwa lugha ya Kiingereza Aprili 27, 2023 kama makala ya jarida la Mokoro Kwa idhini ya mwandishi. 

Comparta esta página